SAKATA
la usajili wa mchezaji Shafii Hassan aliyesajiliwa na Simba SC kutoka
Zimamoto, limechukua sura mpya baada ya klabu ya Malindi SC kuibuka na
madai kwamba mchezaji huyo ni mali yao.
Katibu
Mkuu wa Malindi Mohammed Masoud Rashid, ameiambia BIN ZUBEIRY leo
kwamba si Zimamoto wala Ashanti United yenye haki ya kumtumia au kumuuza
mwanasoka huyo.
Kwa
hivyo, Malindi ameitahadharisha Simba kutokufanya kosa, na kama
inamtaka beki huyo inalazimika kufanya mawasiliano na uongozi wa timu
hiyo na kufuata taratibu za usajili.
Masoud
alieleza kushangazwa na hatua ya Simba kudai kuwa wamemsajili mchezaji
huyo kutoka Ashanti United, wakati klabu anapaswa kuhamishwa kutoka
Malindi.
Katibu
huyo alidai kuwa, Shafii ana mkataba wa miaka miwili klabu yake ambao
bado haijamalizika, hivyo kitendo cha Ashanti United msimu uliopita
kumsajili, hakikuwa halali.
Masoud
alisema usajili huo ulifanywa kwa mabavu na Chama cha Soka Zanzibar
(ZFA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na
kusisitiza kuwa ni vyema Simba iwasiliane na uongozi wa Malindi yenye
mkataba na mchezaji huyo.
"Tunaitahadharisha
Simba kwamba Shafii ni mchezaji wetu na si wa Zimamoto wala Ashanti.
Ssisi hatutaki ugomvi nao lakini kama hawakuja kumsajili kwetu tupo
tayari kwenda popote kudai haki yetu," alisema Masoud.
Masoud
alidai hiyo si mara ya kwanza Simba kuwatenda kwani walishawahi
kumnyakua kijanja mchezaji wao Adeyoum Saleh, lakini wakawaachia kwa
kuwa hapo mwanzo walikuwa na udugu mzuri.
"Aliposajiliwa
Shafii Ashanti tulipeleka malalamiko ZFA, lakini wakaamua kutupuuza,
hivyo tunaamini alisajiliwa kwa matakwa na maslahi ya viongozi wa ZFA na
TFF kwa kutumia vyeo vyao," alidai.
Katibu
huyo alifika mbali zaidi kwa kutamka wazi kwamba timu ya Zimamoto
inahusika kwa kiasi kikubwa katika kumtorosha mchezaji huyo kwenda
Ashanti, ili waweze kumsajili kirahisi.
"Katika
hili TFF, ZFA, Zimamoto na Ashanti wote walihusika kumtorosha kwani
tulipowasiliana na TFF kipindi hicho walitujibu kuwa hawawezi
kulishughulikia suala hilo," aliongeza.
Akizungumzia
kadhia hiyo, Raisi wa ZFA Ravia Idarous, ameishangaa Malindi, akidai
kuwa wakati wa dirisha dogo msimu uliopita, mchezaji huyo alichezea
Ashanti hadi mwisho wa ligi, lakini klabu hiyo ilikaa kimya.
Alisema
ZFA ilimuidhinisha mchezaji huyo aliyekuwa huru kuichezea Ashanti baada
ya timu hiyo kukamilisha taratibu zote za usajili, na kwamba hafahamu
Malindi inatumia vigezo gani kudai Shafii ni mali yake.
Naye
Katibu wa Zimamoto Ali Jongo akimshangaa Katibu wa Malindi inapata wapi
jeuri ya kudai mchezaji huyo ni wao, na kuongeza kuwa hawana muda wa
kulumbana, bali wanashughulikia mambo mengine yaliyopo mbele yao.
![]() |
Pingamizi; Beki mpya wa Simba SC, Shaffi Hassan akiwa mazoezi na timu yake mpya |
No comments:
Post a Comment