Wednesday, 3 September 2014

COUTINHO KUENDELEZA MAKALI YAKE LEO TAIFA?


KIUNGO mpya wa Yanga SC, Mbrazil Andrey Coutinho aling’ara katika mechi za kirafiki za timu hiyo visiwani Zanzibar akifunga mabao mawili katika michezo mitatu. Na alifunga mabao mazuri Uwanja wa Amaan, Zanzibar moja kila mchezo, Yanga SC ikishinda 2-0 mara zote dhidi ya Shangani na KMKM. Zaidi ya kufunga mabao, Coutinho alionyesha uwezo mkubwa mno wa kucheza soka- kwa ujumla umiliki wa mpira, kasi, utoaji wa pasi, upigaji krosi, kona na mashuti ya mbali. Alionyesha uwezo wa kupasua katikati ya wachezaji wa timu pinzani na kufumua mashuti ya kushitukiza na kufunga mabao yake hayo mawili mazuri.
Kifaa cha ukweli; Andrey Coutinho aling'ara na Yanga SC Zanzibar, je leo ataendelea cheche zake Taifa?
Kwa mashabiki wa Yanga SC wa Dar es Salaam waliosikia sifa za Coutinho Zanzibar, bila shaka leo itakuwa fursa nzuri kwao kujionea wenyewe juu ya Mbrazil huyo. Watapata fursa hiyo wakati Yanga SC ikimenyana na Thika United ya Kenya katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mchezaji mwingine mpya wa Yanga SC kutoka Brazil, Geilson Santana ‘Jaja’ ambaye pamoja na kufunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Chipukizi Uwanja wa Gombani, Pemba hakuvutia sana kiuchezaji, naye atakuwa na nafasi nyingine ya kudhihirisha uwezo wake kwa wana Yanga wa Dar es Salaam.    Kwa ujumla kocha mpya, Mbrazil, Marcio Maximo atahitaji kuendeleza rekodi ya ushindi baada ya kushinda mechi zote tatu za kujipima nguvu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment