Barcelona yaanza LALIGA kwa makeke, Messi ang’ara
Timu ya soka ya Barcelona ya Uhispania imeanza msimu mpya wa ligi
kuu ya soka nchini humo al-maarufu LALILGA kwa ushindi wa mabao 3-0
dhidi ya timu ya Elche. Timu hiyo ambao kwa sasa inanolewa na mkufunzi
Luis Enrique ikicheza katika uwanja wake wa nyumbani wa Camp Nou
ilionekana ikiwa na sura nyingi ngeni baada ya kuwasajili makinda kadhaa
akiwemo Munir El Haddadi mwenye umri wa miaka 18 ambaye anaonekana kuwa
tishio katika safu ya ushambuliaji. Nyota wa timu hiyo Lionel Messi
alipachika mabao 2 katika dakika za 42 na 63, huku bao la tatu likitiwa
kimiani na kinda Munir El Haddadi katika dakika ya 46 ya mchezo. Mambo
yalionekana yangewavurugikia Barcelona baada ya mlinzi wake Javier
Mascherano kulimwa kadi nyekundu katika dakika ya 43 ya kipindi cha
kwanza. Hata hivyo pengo la Mascherano halikuwa kikwazo kwa Barcelona
kung’ara na kuibuka na ushindi katika mchezo huo. Katika mechi nyingine
za ufunguzi zilizochezwa jana Celta de Vigo imeibamiza Getafe mabao 3-1,
Villareal imeitandika Levante viboko viwili bila majibu, Granada
imeipeleka mchakamchaka Deportivo de la Coruna kwa kuifunga mabao 2-1,
Malaga imeiadhibu Athletic bao 1 kwa yai, huku Sevilla na Valencia
zikitoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1, matokeoa ambayo yalitawala pia
mchezo kati ya Almeria na Espanyol. Ligi hiyo itaendelea tena leo ambapo
Real Madrid watamenyamana na Cordoba huku mabingwa watetezi Atletico
Madrid wakiwa wageni wa Rayo Vallecano.
No comments:
Post a Comment