Katika safu ya wanaspoti waliokuwa kwenye viti vya magurudumu katika mchezo huo wa kabadde, Thakur Vinod wa India alishinda dhahabu kwa kupata pointi 206. Muirani Shahabedin Basamtabar aliibuka wa pili kwa kupata pointi 149 na kujishindia medali ya fedha, kando na medali ya dhahabu aliyoishinda hapo awali. Asadullah wa Pakistan aliyeibuka wa tatu alijishindia medali ya shaba kwa kupata pointi 109.
Timu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa kupata jumla ya pointi 39 ikifuatiwa na Pakistan na Tajikistan zilizopata pointi 33 na 31 mtawalia. India imeboronga katika mashindano hayo na kuvuta mkia.
Wanamichezo kutoka nchi hizo 4 za bara Asia wameshiriki duru ya kwanza ya Mashindano hayo ya Michezo ya Kunyoosha Viungo ya Bara Asia kwa Walemavu maarufu kama Parazurkhaneh yaliyofanyika katika ukumbi wa Abul Qasim Firdaus mjini Dushambe nchini Tajikistan.
Ligi Kuu ya Soka ya Iran
Klabu ya Esteqlal imeendelea kujikita kileleni mwa Ligi Kuu ya Soka ya Iran baada ya kuichachafya Naft ya Tehran mabao 2-0 katika uwanja wa Azadi hapa jijini Tehran, siku ya Jumamosi. Katika mchuano huo uliokuwa wa kisisimua wa wiki ya 17 ya Ligi Kuu ya Soka hapa nchini, kiungo Andranik Teymourian aliipa Esteqlal bao la kwanza kunako dakika ya 32. Esteqlal iliendelea kuwa kifua mbele hadi timu mbili hizo zinaenda mapumzikoni. Katika kipindi cha pili, timu hizo zilibanana lakini dakika tatu kabla ya kulia kipenga cha kuhitimisha mchezo, Hanif Omranzadeh alifunga bao safi la kichwa akiunganisha krosi iliyochongwa na Mojtaba Jabbari na kuihakikishia Esteqlal pointi tatu muhimu.
Kwa ushindi huo, Esteqlal inasalia katika nafasi ya kwanza ya msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33, ikifuatiwa na Sepahan na Naft ya Tehran ambazo zina pointi 30.
Spoti Afrika
Hatimaye al Shabaab yaruhusu soka lakini kwa masharti
Kundi la wanamgambo wa Somalia la al Shabaab limeruhusu soka kuchezwa nchini humo, lakini limeweka sharti kuwa vazi la suruali ndiyo livaliwe na wachezaji wakati wa mechi. Kundi la al Shabaab lenye misimamo mikali limeruhusu soka kuanza kuchezwa katika eneo la Shabelle ambalo linalidhibiti.
Mechi ya kwanza chini ya amri hiyo ilikuwa wakati FC Sahan ilipochakazwa na Balguray mabao 4-0 wikendi iliyopita chini ya usimamizi wa viongozi wa al Shabaab.
Ni mara ya kwanza baada ya miaka miwili kwa soka kuchezwa katika eneo hilo baada ya kundi hilo kuupiga marufuku mchezo huo kwa madai kwamba, ulikuwa kinyume cha maadili ya dini ya Kiislamu.
Timu zinazoshiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Sahan, Bal-Guri, Horseed, Dekedaha, Elman, Sanai, Bulo-Sheikh na FC Nasiib.
Hata hivyo, kundi hilo lilitoa masharti ya kutoruhusu kuandikwa majina ya wasiofuata dini ya Kiislamu kwenye jezi za timu.
Wachezaji wanatakiwa kuvaa suruali na kusimamisha mechi pale inapofika muda wa kuswali.
Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza; Gunners yashindwa kutamba mbele ya City
Manchester City siku ya Jumapili walionyesha tena ari na nia yao ya kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza msimu huu, kwa kuisasambua Arsenali goli 1-0. Kufuatia majirani Man United awali kuifunga QPR magoli 2-0, Man City ilifahamu lazima iwike nyumbani na haikupoteza fursa hiyo. Katika dakika ya 53, David Silva alitia kimyani bao hilo ambalo liliitosheleza City kusalia kileleni mwa ligi. Awali, mkwaju mkali wa Mario Balotelli haukuweza kufua dafu, licha ya kuuelekeza vyema mpira wavuni. Sergio Aguero alikuwa na nafasi ya kuongeza idadi ya mabao, lakini mpira wake ulipaa juu mno, huku Pablo Zabaleta naye akigonga mwamba. Lakini Gunners hawawezi kulalamika kwamba hawakupata nafasi ya kufunga mabao, kwani kipa Joe Hart aliweza kuiokoa timu yake kutokana na mikwaju ya Gervinho, Theo Walcott na Aaron Ramsey.
Hadi sasa, Man City inadumisha rekodi ya kutoshindwa katika uwanja wa nyumbani wa Etihad msimu huu, kwa asilimia 100. Kati ya mechi 28 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Man City imeondoka na sare katika mechi mbili tu.
Katika viwanja vingine, Aston Villa ilishindwa magoli 2-0 ilipocheza na Liverpool. Tottenham nayo inashikilia nafasi ya tatu katika Ligi ya Premier, baada ya kuifunga Sunderland bao 1-0.
Jordi Gomez alisawazisha katika dakika 87 na kupunguza kasi ya Chelsea katika juhudi za kufikia kilele cha Ligi Kuu ya Premier na kuiwezesha timu yake ya Wigan kupata pointi muhimu katika kujinusuru kusalia katika ligi.
Kwengineko, Blackburn ilishindwa magoli 2-1 ilipocheza na West Brom wakati Everton ikilazimishwa sare ya 1-1 ilipokutana na Norwich. Fulham ilithibitisha ngome ya Bolton bado ni dhaifu kwa kuwafunga magoli 2-0 kwa kirahisi. Stoke iliishinda Wolves mabao 2-1 huku mechi moja tu wikendi hii ikikosa mabao, ile kati ya Newcastle na Swansea. Barca Watamba tena Kombe la FIFA la Vilabu
Barcelona wameshinda Kombe la Dunia la Shirikisho la Soka Duniani FIFA kwa vilabu baada ya kuicharaza timu ya Santos ya Brazil mabao 4-0 kwenye mchezo wa fainali uliyochezwa nchini Japan. Ushindi huo umeendeleza rekodi nzuri ya klabu hiyo kwa mwaka huu ambapo wao ni mabingwa wa Ligi ya Hispania maarufu kama La Liga. Aidha, Barca wanashikilia ubingwa wa Vilabu vya Ulaya na pia Kombe la Hispania maarufu kama Spanish Super Cup. Mpachika mabao wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi aliifunga Barca mabao mawili, huku mengine yakiwekwa kimiani na Xavi pamoja na nahodha na kiungo wa zamani wa Arsenal Cesc Fabregas. Ushindi huo unathibitisha kwamba Barcelona inaendelea kusalia timu bora ya kusakata kandanda duniani.
Uislamu na Michezo
Wiki iliyopita, safu hii iliendelea kukutajieni baadhi ya faida zinazopatikana kutokana na mchezo wa kukimbia au kutembea masafa marefu. Katika kutamatisha kuwadondoleeni baadhi ya faida na umuhimu wa mchezo huo, Sheikh Siraj Henricks anasema kuwa, kiafya, kukimbia kunaongeza nguvu na nishati mwilini. Inasemekana kuwa, kukimbia asubuhi kunaupa mwili nishati mchana kutwa na kukimbia nyakati za jioni kunafungua viungo na kumfanya mtu kuwa na usingizi mwanana usiku kucha. Wataalamu wa afya wanasema kuwa, kukimbia kunamfanya mtu ajiamini na kuwa na ari ya kutekeleza vyema mambo yake. Nukta nyingine muhimu kuhusiana na haya ni kuwa, kukimbia au kutembea kwa masafa marefu kunampunguzia mtu msongo wa mawazo na fikra nyingi. Pamoja na faida, umuhimu na nukta zote tulizokudondoleeni katika kipindi cha leo na vipindi vilivyopita, mchezo huo hauna gharama wala kuhitaji maandalizi na ujuzi wowote. Mtu anaweza kukimbia au kutembea kwa masafa anayoweza, popote pale alipo na muda wowote ule.
No comments:
Post a Comment