MIDO LA UKWELI JONAS GERARD MKUDE SASA FITI KABISA, KUINGIA KAMBINI JUMTATU ZENJI SIMBA SC
KIUNGO
wa kimataifa wa Tanzania, Jonas Gerard Mkude ameanza mazoezi mepesi
kuelekea kurejea uwanjani baada ya kupona maumivu ya goti, aliyoyapata
Juni mwaka huu.
Mkude
aliumia akiichezea timu ya taifa, Taifa Stars katika mchezo wa kirafiki
nchini Botswana mjini Gaborone na baada ya vipimo na tiba, akatakiwa
kupumzika kwa wiki sita.
“Nipo
fiti kabisa kwa sasa, nimeanza mazoezi ya viungo chini ya usimamizi wa
Daktari na ninaendelea vizuri,”amesema kiungo huyo wa Simba SC.
Mchezaji
huyo mahiri wa sehemu ya kiungo wa ulinzi, amesema Jumatatu anatarajia
kujiunga na wachezaji wenzake wa Simba SC kambini visiwani Zanzibar.
Atakaporejea,
mtihani wake wa kwanza Mkude utakuwa kujifua kurudi katika kiwango
chake na baada ya hapo amshawishi kocha Mzambia, Patrick Phiri
kumrejesha kwenye kikosi cha kwanza.
Phiri
amerejea Simba SC kipindi ambacho Mkude ni majeruhi, hivyo hajawahi
kufanya naye kazi na tayari amemuamini kiungo mpya Mrundi, Pierre
Kwizera katika nafasi ya kiungo mkabaji.
Lakini
bado mbele ya wana Simba SC, Mkude ndiye mchezaji anayekubalika zaidi
kuzungusha dimba la chini- hivyo kiungo huyo atalazimika kumshawishi na
kocha Phiri akubaliane naye.
Mkude
anaweza kukosa mechi za mwanzo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
ambayo inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu, Simba SC ikifungua
dimba na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Septemba 21.
Mabingwa
watetezi, Azam FC wataanza na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex,
Chamazi, Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu, wakati Yanga SC
waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro siku hiyo.
Washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20.
Mechi
nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United
watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga,
Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na
Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi
mkoani Pwani.
![]() |
Anarudi; Kiungo Jonas Mkude ameanza mazoezi mepesi na Jumatatu anaingia kambini Simba SC |
No comments:
Post a Comment